By Nasibu Mahinya
- Hutumika kutengeneza mafuta ya kupikia.
- Maua yake ni kivutio kwa watalii.
- Ni fursa ya kukuza kipato kwa vijana na wanawake.
Wanasema bustani haikamiliki bila maua na huo ni ukweli usiopingika, maua huongeza mvuto na maua mengine yana tija kwenye lishe yetu pia.
Napenda nikujuze kuwa zaidi ya asilimia 99 ya matunda yote duniani hutokana na maua.
Moja ya vigezo vyangu vya kutafuta mke wa kuoa ni kuwa mwanamke lazima apende na ajue jinsi ya kuhudumia bustani ya maua, tena akiweka na maua ya alizeti atanifurahisha sana.
Je, Alizeti ni ua? Lina upekee gani katika sekta ya kilimo na utalii? Twende pamoja.
Asili ya ua la alizeti ni kaskazini mwa Amerika na lilikuwa likiota kama ua pori huku likitoa bidhaa kama dawa na mafuta hadi kuanza kulimwa kibiashara miaka ya 1500 na wazungu waliolowea Marekani na mwishowe ua hilo kusambaa duniani kote.
Ua hili lenye muundo wa kisahani, lina rangi ya njano kwenye petali na kahawia iliyokolea katikati kwenye mbegu. Ua hili kwa Kiingereza linaitwa ‘Sunflower’ na ni kutokana na sura yake kufanania muonekano wa jua.
Lakini pia kwa kifaransa linaitwa ‘Tournesol’ ikimaanisha ‘kugeukia jua’ ambayo ni sifa nyingine ya ua hili. Ua hili lina uwezo wa kugeukia upande ambao mionzi ya jua hutokea.
Sifa kuu za alizeti
Mmea wa alizeti unaweza kuwa na urefu wa hadi futi 12, sawa urefu wa watu wawili kwenda juu. Alizeti refu kuliko duniani lilikuwa na urefu wa futi 30, lilioteshwa nchini Ujerumani.
Katikati ya ua la alizeti kuna mbegu zisizopungua elfu moja, mbegu hizo ambazo zikikamuliwa hutoa mafuta ya kupikia ya alizeti yenye vitamin A na D na yasiyo na lehemu, yani Kolestro.
Kazi ya alizeti katika shughuli mbalimbali
Alizeti ambalo limeshavunwa mbegu linaweza kutumika kama dodoki la kujisugulia mwili wakati wa kuoga.
Alizeti pia hufanya kazi nzuri ya kunyonya miyonzi ya sumu iliyomo kwenye hewa na kwenye udongo. Kwa mfano, nchini Japan zaidi ya mimea ya alizeti ilipandwa ili kupambana na mionzi ya nyuklia baada ya Tsunami kubomoa matenki ya uranium kwenye kitongoji cha Fukushima mwaka 2011.
Alizeti linavutia sana nyuki hivyo kama mfugaji wa nyuki akipanda maua haya yanaweza kumuongezea faida katika mavuno yake ya asali.
Alizeti ni zao linalovutia watalii
Maua ya alizeti ni kivutio cha watalii hasa wanaopenda kupiga picha zenye maua yanayovutia.
Barani Afrika, zao la alizeti lililetwa na wakoloni na Tanzania ni moja ya nchi 10 duniani zinazoongoza kwa uzalishaji wa zao hili ambapo zaidi ya tani laki tatu huvunwa kila mwaka.
Katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Iringa, Singida na Kilimanjaro ni baadhi ya sehemu ambazo maua haya hupatikana kwa wingi, lakini je, alizeti na muonekano wake wa kuvutia linaishia tu kuwa zao la kibiashara alafu basi?
Nchi kama Marekani na Ukreini ni moja kati ya nchi za kwanza zilizoona fursa ya utalii ndani ya ua la alizeti.
Kwa kuwa maua haya yanavutia machoni na watu wakipiga nayo picha hupendeza, basi mataifa hayo yamebuni aina ya utalii uitwao utalii wa kilimo yaani ‘Agritourism’ ambao unahusisha watalii kutembelea mashamba yakiwemo ya alizeti, kujionea jinsi kilimo hicho kinavyofanywa na pia kupiga picha ambazo zitabakia kuwa kumbukumbu za kudumu milele.
Utalii wa alizeti pia huangukia kwenye utalii wa maua kama ambao yaliyopo kwenye hifadhi ya Taifa ya Kitulo japokuwa maua ya hifadhi hiyo ni uoto wa asili.
Je, wewe ni mkulima wa alizeti na ungependa kupata watalii watakaolipia ziara za shambani kwako? Fursa iko wazi hiyo!