By Maureen C. Minanago.

Wema ni tabia njema inayodhihirisha moyo wa upendo, huruma, na utu kwa wengine. Ni hali ya kuwa mwema kwa maneno na matendo, kuonyesha fadhila na kusaidia wengine bila kutarajia malipo. Kutenda wema ni vitendo vyenye nia njema vinavyolenga kuleta faraja, furaha, na maendeleo kwa mtu binafsi au jamii kwa ujumla.

Namnukuhu Roy T. Bennett anasema, “Daima tafuta fursa kumfanya mwingine atabasamu na kumtendea matendo ya wema kila siku”.
Katika maisha ya kila siku, kutenda wema kunaweza kujidhihirisha kwa njia nyingi, kama vile kusaidia wahitaji, kusema maneno ya faraja kwa waliovunjika moyo, kusamehe waliokosea, na kushiriki rasilimali na wengine kwa hiari. Wema hauna mipaka ya rangi, dini, wala hadhi ya kijamii, bali ni kiungo kinachounganisha wanadamu kwa msingi wa upendo na mshikamano.

Charles Glassman anasema, “Wema huanza kwa uelewa kuwa sote tunapambana”. Waswahili husema mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu. Utambuzi wa kuwa sote ni wahanga kwa namna moja au nyingine hurahisisha kufahamu hisia za mwingine na hivyo kumtendea wema.
Kufanya wema huleta manufaa si kwa yule anayepewa tu bali pia kwa anayetoa. Hii ni kwa sababu moyo wa ukarimu hujenga furaha ya ndani na kuimarisha uhusiano mwema kati ya watu. Pia, jamii yenye watu wema huwa na mshikamano, amani, na maendeleo endelevu kwa sababu watu huishi kwa kusaidiana na kuheshimiana.

Muigizani maarufu kwa jina la Jackie Chan anasema, “Wakati mwingine matendo ya wema na kujali tu ndio hubadilisha maisha ya mtu”.
Katika mafundisho ya dini na falsafa mbalimbali, wema umepewa kipaumbele kama msingi wa maisha yenye baraka. Hadithi nyingi huthibitisha kuwa wema haumpotei mtu, bali humrudia kwa namna moja au nyingine. Kwa hivyo, kila mmoja anapaswa kufanya jitihada za kuwa mwema na kutenda wema bila kuchoka, kwani dunia inahitaji zaidi watu wenye mioyo safi na nia njema kwa wenzao.
Katika hitimisho, kutenda wema si jambo linalohitaji utajiri au uwezo mkubwa bali moyo wa kusaidia na kujali. Hata tabasamu, neno la faraja, au tendo dogo la huruma linaweza kuwa msaada mkubwa kwa mwingine. Tukizingatia kutenda wema kila siku, dunia yetu itakuwa mahali bora pa kuishi. Nasi MBS Trinity Care tuko kuhakikisha tunakujali na kukutendea wema ili kusambaza upendo na kubadilisha maisha ya wengi kwani wema ni mkuu.