Pundamilia: Mnyama Mwenye Rangi Zenye Utata

By Nasibu Mahinya

Siku ya kwanza namuona pundamilia ilikuwa mwaka 2002 kwenye banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika viwanja vya maonyesho ya biashara maarufu kama Sabasaba, jijini Dar es Salaam. 

Nilikuwa nimeongozana na mama yangu mzazi ambaye alikuwa amenishika mkono kikakamavu huku nikitamani japo kuigusa ngozi ya mnyama huyo kwa sababu ilinivutia kuliko kawaida.

Kwa bahati nzuri au mbaya, sikupata ruhusa ya kumshika na wala hata pundamilia mwenyewe asingekubali kushikwa na binadamu yeyote yule kwa sababu mnyama huyu anasifika kwa hulka ya woga.

Ndugu msomaji, mimi nina swali kwako, pundamilia ni mnyama mweusi mwenye mistari myeupe au ni mnyama mweupe mwenye mistari myeusi?. 

Tafakari kidogo. 

Tayari? 

Ok, vizuri! 

Kama umewahi kusikia msemo usemao shukrani ya punda ni mateke, basi utafahamu dhahiri kuwa wanyama hawa wa jamii ya farasi na punda wana nguvu za ziada kwenye miguu yao.

Sasa tuanze kwa kumuelewa vyema kabisa mnyama pundamilia kisha baadae nikupe majibu ya hilo swali.

Pundamilia ni mnyamapori jamii ya farasi ambaye kitaalamu huangukia kwenye familia ya kinasaba kiitwacho ‘Ekwidae’ pamoja na farasi na punda. 

Aina za pundamilia: 

Kuna aina tatu za pundamilia zijulikanazo kitaalamu.

Aina ya kwanza ni Pundamilia Grevi. Pundamilia hawa wana nguvu na ni wapole mithili ya punda na hapo zamani walitumika kubeba mizigo na kuvuta maguta. Wana umbo kubwa kuliko aina nyingine za pundamilia na huishi zaidi kwenye maeneo yenye ukame.

Pundamilia wa milimani ni aina yao ya pili. Hawa ni pundamilia ambao huishi milimani kama jina lao lilivyo. Wana umbo dogo kuliko aina zote za pundamilia na hawana mistari tumboni. Pundamilia hawa huishi kwenye makundi madogo na mara nyingi dume humiliki majike kadhaa na kuishi nao huku madume wengine wakijitenga katika makundi yao.

Aina nyingine ni pundamilia wa Savanna. Hawa ni pundamilia wanaoishi kwenye maeneo tambarare na ndiyo aina ya pundamilia wanaopatikana kwa wingi kuliko aina zote. Pundamilia hawa hupatikana kwa wingi kwenye mbuga na hifadhi zetu za Taifa. Wengi wao wana mistari hadi tumboni.

Binadamu wameshajaribu sana lakini pundamilia hafugiki.

Muonekano wake halisi:

Ukweli ni kwamba pundamilia ni mnyama pori mweusi mwenye mistari myeupe kwa kuwa ngozi yake ni nyeusi iliyofunikwa na manyoya meusi na meupe. Pundamilia akinyolewa manyoya yake anabakia kuwa kiumbe mweusi. 

Pundamilia anaweza kuwa na rangi nyeupe au kahawia iliyofifia pale mazingira yanapochangia kupauka huko au anapokuwa na ulemavu wa ngozi.

Kama zilivyo alama za vidole vya binadamu, huwezi kukuta pundamilia wawili wanafanana, hata pundamilia pacha hawafanani. 

Pundamilia huwa na uzito wa kuanzia kilo 200 mpaka kilo 400 na hii humfanya kuwa chakula pendwa cha wanyama wawindaji kama chui na simba kwa sababu ya kuwa steki ni ya kutosha. 

Maisha yake:

Kwa wastani mnyama huyu huishi miaka 20 mpaka 30 na ndama wa pundamilia huweza kutembea dakika takribani 20 baada ya kuzaliwa na hupata uwezo wa kukimbia baada ya saa kadhaa tu. 

Pundamilia hukimbia kasi ya kilomita 60 kwa saa, hii inamaanisha kama akiamua kusafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Bagamoyo kwa kasi hiyo atatumia muda wa takribani saa moja.

Pundamilia anapoona hatari, njia yake ya kwanza ya kujilinda ni kukimbia. Njia ambayo mara nyingi huwa haimsaidii kwa sababu wanyama wawindaji kama simba, chui, duma na mbwa mwitu wote wana kasi kuliko pundamilia. 

Hapo unapata kuelewa kwa nini pundamilia ni kitoweo pendwa mbugani ukilinganisha na swala ambaye ni moja kati ya wanyama 10 wenye kasi zaidi ardhini au nyati ambaye simba wenyewe wakiwa wachache hawamuwezi kutokana na nguvu alizonazo ng’ombe pori huyo.

Pundamilia hawa hupatikana kwa wingi kwenye mbuga na hifadhi zetu za Taifa. Wengi wao wana mistari hadi tumboni.

Tabia na hulka yake:

Kila mwaka zaidi ya pundamilia 200,000 huhama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara iliyopo nchini Kenya na msafara huo huongozwa na pundamilia mkongwe zaidi. 

Pundamilia huongozana pia na nyumbu na swala kwenye msafara huo ambao pia wanyama wawindaji huufuata nyuma nyuma kwa siri kwa sababu kama kitoweo kinahama sasa kwa nini na wao wasikifuate kilipo.

Zaidi ya simba 3,000 hufuatilia msafara huo kwa umakini sana. Pundamilia hujikusanya kwa makundi kwa ajili ya kujilinda na wanyama wakali porini. 

Kujikusanya kwao pamoja huwafanya wanyama kama simba kutoona vizuri viungo vya miili ya pundamilia, hivyo pale anapojichanganya katikati ya kundi la pundamilia hukutana na mateke ambayo yanaweza kumfanya apoteze maisha.

Kama umewahi kusikia msemo usemao shukrani ya punda ni mateke, basi utafahamu dhahiri kuwa wanyama hawa wa jamii ya farasi na punda wana nguvu za ziada kwenye miguu yao. Kitu ambacho kiliwafanya watu wa zamani kuwaamini wanyama hawa kusafirisha abiria na mizigo kwa umbali mrefu.

Binadamu wameshajaribu sana lakini pundamilia hafugiki. Kitu kimoja ambacho binafsi nilishuhudia na nikastaajabu kwenye hifadhi ya Taifa ya Mikumi ni kwamba pundamilia hulala wima. Mimi nilishajaribu kulala wima, je wewe umeshajaribu? Ukijaribu nijulishe.

Scroll to Top