By Jamal Hamza
Kuamka ukiwa umechoka ni tatizo linalowakumba watu wengi ulimwenguni. Hata baada ya kulala kwa muda unaoonekana kuwa wa kutosha, watu wengi hukosa nguvu na wanakabiliwa na uchovu unaoathiri siku yao nzima. Hali hii inaweza kuhusishwa na sababu nyingi, zikiwemo za kiafya, kisaikolojia, na za mtindo wa maisha.
Cleveland Clinic wameelezea baadhi ya sababu na njia za kuepuka kuamka mchovu au umechoka, na hatua za kushughulikia tatizo hili.
SABABU ZA KUAMKA UMECHOKA
a) Ukosefu wa usingizi wa kina
Usingizi wa kina ni mojawapo ya awamu muhimu zaidi za usingizi. Ni wakati huu ambapo mwili unajirekebisha, seli zinajijenga upya, na mfumo wa kinga unaimarika. Ikiwa usingizi wa kina haupatikani, hata kama umelala kwa saa nyingi, unaweza bado kuhisi uchovu. Hali hii husababishwa na, matatizo ya kiafya kama vile apnea ya kulala (sleep apnea), ambapo njia za hewa hufungika na kusababisha mwili kushindwa kupumzika vyema. Kelele au mwanga mwingi unaokatiza usingizi wa usiku. Matumizi ya kafeini kama vile “Energy Drinks” au pombe kabla ya kulala, ambavyo vinaweza kuathiri ubora wa usingizi.
b) Ratiba mbaya ya kulala
Mwili wa binadamu unategemea saa ya ndani inayojulikana kama circadian rhythm, ambayo inaelekeza muda wa kuamka na kulala. Ikiwa mtu anabadilisha muda wa kulala mara kwa mara au ana tabia ya kulala kuchelewa na kuamka mapema, mwili unakosa utulivu wa kibiolojia. Hii inaweza kusababisha kuamka ukiwa umechoka, hata kama ulilala kwa muda unaoonekana wa kutosha.
c) Msongo wa mawazo na hofu
Msongo wa mawazo ni sababu kuu ya kuamka ukiwa mchovu. Wakati akili yako imezidiwa na mawazo mengi, mwili hutengeneza homoni za dharura kama cortisol. Hii huathiri ubongo na kuzuia mwili kuingia kwenye awamu ya usingizi wa kina. Pia, watu wenye mawazo mengi mara nyingi huamka usiku wakihisi wasiwasi, jambo linalozidisha uchovu.
d) Sababu za kiafya
Magonjwa fulani yanaweza kuathiri uwezo wa mwili kupumzika vyema wakati wa usiku. Baadhi ya magonjwa haya ni:
- Upungufu wa madini ya chuma (anemia): Hali hii husababisha mwili kuwa na viwango vya chini vya oksijeni, na hivyo mtu kuhisi mchovu kila wakati.
- Matatizo ya tezi (hypothyroidism): Tezi za mwili zinapokuwa dhaifu, zinaweza kusababisha hali ya uchovu wa kudumu hata baada ya kulala.
- Upungufu wa maji mwilini: Mwili unapokosa maji ya kutosha, unaweza kuhisi uzito na uchovu hata baada ya usingizi.
2. NJIA ZA KUEPUKA KUAMKA UMECHOKA
a) Kuanzisha ratiba na mazingira bora ya kulala
Mwili unajisikia vyema unapokuwa na ratiba ya kulala na kuamka thabiti. Hakikisha unalala na kuamka kwa wakati uleule kila siku, hata wikendi. Unda mazingira bora, ya kulala mazoezi ya kulala katika mazingira bora ni muhimu. Epuka mwanga mkali na kelele, vaa mavazi yanayofaa na hakikisha chumba chako kina joto linalofaa.
b) Punguza Msongo wa Mawazo
Mbinu za kuepukana au kupunguza msongo wa mawazo zipo nyingi sana. Jifunze mbinu za kupunguza msongo wa mawazo kama vile kufanya mazoezi, kupumua kwa utulivu, kusoma vitabu au hata kusali.
e) Kula na kunywa kwa afya
Lishe bora ina mchango mkubwa. Hakikisha unakula chakula chenye virutubishi muhimu na unakunywa maji ya kutosha ili kuepuka upungufu wa maji mwilini.
Nimalize kwa kusema, kuamka ukiwa umechoka ni dalili ya matatizo yanayohitaji kushughulikiwa kwa makini. Kwa kuelewa sababu za tatizo hili na kuchukua hatua thabiti, unaweza kuimarisha ubora wa maisha yako. Hakikisha usingizi wako unakuwa kipaumbele, kwani ni msingi wa afya bora, furaha, na uzalishaji wa kila siku.