By Nasibu Mahinya
- Mbuyu ni ishara ya maisha kwa binadamu na wanyama.
- Ina uwezo wa kuishi zaidi ya miaka 1500.
- Upekee wake hutoa tafsiri mbalimbali duniani.
Mbuyu ni mmea unaobeba kumbukumbu nyingi sana za maisha yetu ya utotoni. Shule ya msingi niliyosoma ilikuwa na mbuyu katikati ya eneo ambalo limezungukwa na majengo ya madarasa.
Tukishaangalia filamu za kutisha na tukishaanza kusimuliana hadithi hizo kuhusu mti huu, hatimaye nikatokea kuuogopa na kuanza kupita mbali na nao.
Wengi walikuwa wakihadithiana kuhusu mibuyu inavyotumika kwenye visa vya filamu za kutisha vinavyohusika na kuwafanya watazamaji kuamini kuwa miti hiyo inahusika na nguvu za giza.
Siku hizi nimeshakuwa mtu mzima, naweza kulala peke yangu kwenye tawi la mbuyu usiku mnene peke yangu kwa sababu nimetokea kuujua vizuri mti huu na kutambua kwamba mbuyu ni mti unaohusishwa na uhai huko mbugani.
Mbuyu ni ishara ya maisha kwenye tambarare za barani Afrika na ni baba ya vichaka huko mbugani na unaweza kusema ni moja ya miti mikubwa zaidi duniani.
Kuna aina tisa za mibuyu, aina mbili tu hupatikana barani Afrika ambazo kisayansi huitwa Adansonia Digitata na Adansonia Kilima huku aina moja ikipatikana barani Australia na sita zingine zikipatikana kisiwani Madagascar.
Mti wa mbuyu una urefu wa kufikia mita 25 (sawa na jengo lenye ghorofa 6) na upana wa takribani mita 45 kama ukiamua kuuzunguka.
Mibuyu pia inapatikana kwa wingi zaidi nchini Australia na imekuwa ikipandwa nchi zingine kama India, China na Oman na ina uwezo wa kuishi zaidi ya miaka 1500. Uhai wa mbuyu ni wa kudumu vizazi vingi.
Mibuyu huonekana kuwa miti iliyogeuzwa juu kuwa chini na chini kuwa juu kwa sababu kipindi cha msimu wa vuli, ambapo miti hupukutisha majani yake na kuacha matawi yake yakionekana kama mizizi. Hii hutokea kipindi kuanzia mwezi wa tatu hadi wa tano.
Mbuyu una manufaa mengi kwa binadamu na ndiyo maana ukapewa jina la ‘Mti wa Maisha.’
Mbuyu ni mti unaotunza kiasi kikubwa cha maji, zaidi ya asilimia 60 ya shina la mbuyu ni maji. Mbuyu unaweza kutunza zaidi ya lita 4,000 za maji, hilo si tenki kabisa.
Mbuyu unapozeeka, uwezo wake wa kutunza maji hupungua kwa kiasi kikubwa na kusababisha kukauka kwa sehemu ya katikati ya shina lake ambapo huacha kama uwazi.
Uwazi huo unaweza kutumika kama sehemu ya kujihifadhi na kupata usingizi wako mzuri lakini pia sehemu zingine wameweza kuutumia uwazi huo kiubunifu kwa kuifanya kuwa sehemu ya kuuzia vinywaji.
Mabanzi na mbao za shina la mbuyu ni malaini na yenye nyuzi hivyo yana sifa kudhibiti moto kwa hiyo mbuyu hauwezi kuungua. Pia nyuzi hizo zinaweza kutengenezea bidhaa kama kamba na nguo. Bidhaa zingine zitokanazo na mbuyu ni sabuni, gundi, mpira na dawa za asili.
Mbuyu kuitwa mti wa maisha pia hutokana na uwezo wake wa kuwapa wanyamapori hifadhi kwa ajili ya kulala au kupumzika, kuanzia mnyama mdogo kama mjusi hadi mnyama mkubwa kama tembo wote hupata hifadhi mbuyun
Tunda la mbuyu, lina rangi ang’avu ya mahameli ama ‘velvet’ na lina mbegu nyeusi ambazo zimezungukwa na unga mweupe ambao hutumika kutengeneza kinywaji safi kabisa cha ubuyu.
Unga huo pia unasaidia kuboresha afya ya ngozi, moyo na kusaidia kupungua kwa uzito mwilini.
Tunda la mbuyu lina virutubisho vingi kama madini ya chuma, kalshiamu na potashiamu ambavyo vina kiwango mara mbili zaidi ya vile vya kwenye mchicha. Baadhi ya ripoti zinasema ule unga wa tunda la mbuyu una vitamini C mara 10 zaidi ya chungwa.
Aidha pia, mbegu za tunda la mbuyu ndiyo hutumika kutengeneza kiburudhisho cha kumung’unya kiitwacho ubuyu.
Majani ya mbuyu yamekuwa yakitumika kama mboga na baadhi ya jamii za barani Afrika.
Dhana mbalimbali kuhusu mbuyu
Mbuyu unahusishwa na stori nyingi sana za kufikirika. Kuna baadhi ya watu huamini kwamba kuna shughuli za kishirikina huendelea ndani ya mibuyu au labda ni sehemu wa washirikina kupumzika.
Zamani za kale,hadithi zingine zilisambaa kwamba kuna mbuyu uliwahi kuwataka kimapenzi mabinti wa kijiji kiasi cha kwamba kila muda mabinti hao wakipita karibu, mbuyu huo ulidondosha matunda na kupuliza upepo mzuri na kuwapa kivuli lakini jitihada za mbuyu kuwavutia mabinti hao zikagonga mwamba.
Licha ya mbuyu kuonyesha upendo wote huo, mabinti hao walijiingiza kwenye mahusiano na wanaume wa kijiji na siku moja mabinti hao waliaga majumbani kwao kwenda kutembea na hawakurudi tena, ikisadikika mbuyu huo uliwafungia ndani ya shina lake milele kama kisasi.
Wengine waliamini pia kwamba watoto wakipotea kishirikina basi hukutwa wamerejeshwa chini ya mbuyu lakini pia waliamini kwamba kumuogesha mtoto chini ya mbuyu humsaidia kukua na kuwa mwenye nguvu kama mbuyu.
Iliaminika pia kwamba wanawake waliyoishi kwenye maeneo yenye mibuyu wana uwezo mkubwa wa kupata uja uzito kuliko wale wanaoishi maeneo yasiyo na mibuyu.
Na pia ni tamaduni mpaka leo kwamba eneo lenye mti mkubwa kama mbuyu basi panafaa kuwa sehemu ya jamii au kijiji kukutana na kufanya mikutano ya hadhara.