By Nasibu Mahinya
Tofauti na viumbe wengine, kasuku anaongoza kwa kufugwa na watu katika makazi yao. Kwa miaka mingi, ndege kasuku amekuwa kivutio kwa binadamu kutokana na sifa zake za kipekee. Miaka hivi ya karibuni, tafiti zimegundua kuwa jumla ya idadi ya ndege millioni 14 wanaishi kama mateka nchini Marekani na ndege hao wanasemekana kutoka mabara tofauti na zaidi ya asilimia hamsini ya ndege hao ni kasuku.
Kasuku yupo tofauti na viumbe wengine kwa sababu ndege huyu huishi miaka mingi na ana uwezo mkubwa wa akili. Hivyo basi makala hii itakusaidia kumjua zaidi iwapo kama hukupata nafasi ya kumjua kipindi wengi wakiwa wanamfuga ndege huyu mpiga domo. Uzuri ni kwamba, Kasuku hachagui sana msosi, anakula karibu kila kitu.
Kuna aina nyingi za kasuku
Kuna aina takribani 350 za kasuku duniani wenye rangi za tofauti za kuvutia kama buluu, njano, kijani, nyeupe, nyeusi na nyekundu. Barani Afrika, kasuku wa kijivu ndiyo hupatikana kwa wingi zaidi.
Kasuku wengi hutekwa
Robo tatu ya kasuku wote duniani wapo kwenye hatari ya kupotea kwenye uso wa dunia kwa sababu ya shughuli za binadamu za ukataji miti na biashara haramu ya kusafirisha na kuuza wanyama.
Jike au dume?
Ni ngumu sana kutofautisha kasuku dume na jike, Wanafanana asilimia 99.9. Watu wengi zamani walikuwa wananunua kasuku mtaani alafu wanajikuta wana madume mawili yanatazamana humo bandani.
Mdomo wa ajabu kidogo
Kasuku ana mdomo uliyojikunja kuelekea chini kama mundu na anakula chochote anachokutana nacho kuanzia nyasi, matunda, mbegu, majani, maua mpaka nyama.
Kasuku ana ulimi ambao hautumii kuonja chakula, kazi ya kuonja chakula hufanywa na upande wa juu wa ndani ya mdomo.
Kasuku hata siyo mzito
Kulingana na aina ya kasuku, ndege huyu anaweza kuwa na uzito wa kuanzia gramu 60 mpaka kilo moja na nusu.
Kasuku anakula chumvi nyingi!
Kasuku anaweza kuishi hadi miaka hamsini, na kasuku mzee kuliko wote ana miaka 86 na anaishi kwenye hifadhi iitwayo Brookfield iliyopo mjini Chicago, nchini Marekani.
Kuna watu walifuga kasuku wakaacha migogoro ya mirathi, familia haikujua nani atamrithi huyo ndege. Ya Mungu mengi na miaka 50 ni mingi kweli kweli.
Kasuku ana kinga asilia
Manyoya ya kasuku yana kinga dhidi ya bakteria. Kinga ambayo huwapa manyoya yao rangi nyekundu, kijani na njano.
Hachelewi kuhama kambi
Kasuku huhama pale hali ya hewa inapobadilika kutafuta malisho. Hata kama nyumbani kwako kuna vitu asivyovipenda, usishangae siku moja hujafunga banda vizuri, anaondoka na hutomuona tena.
Kasuku anapiga domo!
Kasuku anapenda sana kupiga domo. Yeye hana uwezo wa kuongea bali ana uwezo wa kukariri maneno yanayosemwa na mwanadamu, hivyo basi kuwa mwangalifu na maneno uyasemayo mbele ya kasuku maana atayarudia tu muda wowote.
Kasuku anayeshikilia rekodi ya dunia ya kujua maneno mengi alikariri maneno 1,700. Ingawa hatuwezi tena kumfuga mjumbani lakini pata picha kasuku kakaririshwa nyimbo afu kapelekwa kuimba kwenye ‘karaoke Raha’ sana!