By Nasibu Mahinya
Inajulikana kwamba fisi akishika windo lake haachi kitu, anakula kuanzia kichwa hadi kwato. Dah! Hongera zake kwa kweli, maana mimi kila nikiwaza ng’ombe anapochinjwa kuna viungo vyake vingi huwa havifiki mezani. Fisi amethibiti upotevu usiyo na tija, wazungu wanaita ‘total diet.’ Hata asiyemjua fisi atakuambia jinsi mnyama huyo alivyopewa sifa ya kula kwenye hadithi na vitabu vingi lakini kama umekuja hapa kusoma hii makala, basi amini kwamba kuna mengi zaidi yatakayokuacha mdomo wazi.
Binafsi kuandika tu hii makala, nikajikuta namshangaa fisi kama simjui vile wakati nishakutana naye mbugani mara nyingi tu; ni muoga tu hana lolote!
Fisi ni mnyama jamii ya paka, ana ngozi ya njano ama kahawia mpauko yenye mabaka meusi. Hupenda kula wanyama wengine na huwinda kwa makundi.
Fisi kala fisi!
Jambo moja la kushangaza ni kwamba fisi anaweza kula fisi mwenzie. Kama vitoto vimezaliwa halafu ndiyo njaa imetawala basi hao ni chakula cha baba, kwani shida iko wapi? Si watazaa tu wengine!!! Na endapo akilipania windo hakubali kushindwa kirahisi, lazima atalipata.
Ikiwa mnyama huyu amekula akashiba atalala lakini ikatokea ghafla wanakikundi wenzake wamemkamata nyumbu lazima ataamka na kujitapisha chakula alichokula ili tumbo lipate nafasi ya kumuweka nyumbu. Ndiyo maisha ya fisi hayo, mdomo ukiwa bize basi kwake yeye ndo ‘kasha-win’ maisha.
Fisi jike ndiye masta, mbabe kuliko dume. Ana umbo kubwa na ni mkali zaidi kwenye suala la uwindaji. Fisi jike na fisi dume wote wawili wana uume. Uume wa dume hutumika katika kujamiiana ambapo huingia ndani ya uume wa jike. Kwa upande mwingine, uume wa jike hutumika kwenye uzazi na huishia kuchanika wakati anazaa.
Katika uzazi, uume wa jike humpitisha mtoto na kwa kuwa ni mdogo basi mtoto wa fisi anaweza kupoteza maisha kwa kukosa hewa wakati anapitishwa kwenye uume huo.
Fisi jike ana chuchu mbili tu ambazo watoto hugombania kunyonya hadi kuuana. Yaani mtoto wa fisi anapitia shuruba nyingi sana mpaka anakuja kuwa mkubwa na ndiyo maana hawezi kukubali kufa kizembe eti fisi afe kwa njaa, kweli!? Wako radhi hata wale viatu vya ngozi vilivyosahaulika na watalii kunusuru uhai, hivyo fisi hujitosa tu.
Inasemekana kuwa fisi ana uwezo wa kufikiria kuliko sokwe. Hupenda kuiba mayai ya wanyama wengine kama mbuni. Yai la mbuni huwa ni ngumu kwa yeye kulipasua kwa meno yake hivyo basi hutafuta bonde lenye mawe au miamba, na yeye akiwa kwenye mwinuko, kisha huliachia yai hilo literemke na kupigiza kwenye mawe na miamba.
Hufanya hivyo mara nyingi mpaka yai lipasuke ili aweze kula kilichomo ndani. Fisi hashindwi kwenye kula.
Ni wanyama wa usiku, wanaishi kwenye nyasi, misitu, vichaka, jangwani na hata milimani. Wanyama hao ni waoga lakini umoja wao huwafanya kumshinda adui kwa urahisi na kula nyama yake bila kusalia kitu.
Ukisikia kicheko porini amini kwamba hapo kuna hatari. Fisi hucheka kama mshangao akiona chakula. Fisi huwinda kwa makundi na fisi mwenye kicheko kikali zaidi ndiyo kiongozi wa kundi; na mara nyingi kundi huongozwa na fisi jike.
Fisi dume hutimuliwa kwenye familia akishafikia balehe na hapo ndipo hujiunga na kundi la uwindaji na ni lazima apigane na fisi dume wa kundi hilo, na muda mwingine hupigana hadi kupoteza maisha.
Fisi ni muoga sana akiwa peke yake, hana ujanja mwingi. Awapo mwenyewe hula watoto wa wanyama karibu wote uwajuao, kuanzia simba, chui, tembo hadi kifaru kwa sababu ana uwezo wa kuwamudu ila wakiwa kikundi wanakuwa na nguvu sana na kujiamini. Kundi la fisi linaweza kupigana na kundi la simba bila uwoga kabisa.
Zamani fisi walikuwa wanahushishwa na ushirikina kwamba wachawi huwapanda kama farasi na kuwatumia kama usafiri wakienda kuiba watoto wa mifugo.
Fisi wanapatikana karibu kila mbuga hapa nchini na kama tulivyosema hapo awali, fisi huishi kwenye nyasi, misitu, vichaka, jangwani na hadi milimani. Tembelea Ngorongoro ujionee kwa macho yako mishemishe za fisi kutafuta mawindo mbugani.
Tukutane tukiwa tumeenda mnara! Fisi hufanya mikutano ya kuwasiliana ambayo majike na madume wote huudhuria huku wakiwa wamesimamisha uume wao. Wanasayansi wanaamini kwamba uume wao huwasaidia kuwasiliana. Binafsi, naomba huu uwe mjadala mpana wa siku nyingine tafadhali. Hahahah! Ahsante.