By JAMES MANJECHE
Vija wanaomaliza masomo yao vyuoni mara nyingi hukutana na hali halisi, tofauti kabisa na matarajio waliyokuwa nayo wakiwa masomoni. Wengi huingia mtaani wakiwa na ndoto kubwa za kufanikisha maisha, lakini changamoto nyingi huwazuia kufikia malengo yao kwa haraka. Mimi kama shuhuda mmoja wapo, vijana wengi tunakumbana na chanagmoto nyingi baada tu ya kutoka vyuoni. Zifuatazo ni baadhi ya changamoto;
UKOSEFU WA AJIRA
Moja ya changamoto kubwa inayowakumba vijana ni ukosefu wa ajira. Wanafunzi wengi huamini kuwa kupata shahada ni tiketi ya moja kwa moja ya kupata kazi nzuri, lakini hali halisi ni tofauti. Uchumi wa nchi nyingi, hasa barani Afrika ikiwemo Tanzania, hauwezi kutoa nafasi za kazi za kutosha kwa wahitimu wote.
UKOSEFU WA UJUZI WA KAZI
Licha ya kuwa na elimu ya darasani, wahitimu wengi wanakosa ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira. Waajiri wengi huweka kipaumbele kwa watu wenye uzoefu wa kazi, jambo linalowaweka wahitimu katika hali ngumu ya kuanza kazi.
Kwa mfano: Waanafunzi wengi wanaomaliza shahada ya biashara katika vyuo vya biashara wanajikuta wakishindwa katika mahojiano ya kazi (Interview) kwa sababu yakutokuwa na uzoefu wa kutosha wa kutumia programu za kifedha ambazo waajiri walihitaji.
KUKOSEKANA KWA MITAJI YA KUANZISHA BIASHARA
Kwa baadhi ya vijana, changamoto ya ajira huwafanya kufikiria kuanzisha biashara zao wenyewe. Hata hivyo, ukosefu wa mtaji huwa kikwazo kikubwa. Hali ya kiuchumi na masharti magumu ya mikopo pia huwazuia vijana wengi kufanikisha ndoto zao za ujasiriamali.
Kwa mfano, wanafunzi wengi huwa na dhana ya kupata ajira mara baada ya kuhitimu elimu ya juu lakini wanajikuta katika dimbwi la wahitimu wasio na ajira hivyo kujiunga na biashara. Isivyo bahatizbiaahara hizo nazo huwa na changamoto ya mtaji wa kuanzisha ama kuendeleza biashara hiyo.
CHANGAMOTO ZA KIAKILI NA KIHISIA
Changamoto za kiakili na kihisia ni tatizo linalowakumba vijana wengi wanaotoka vyuoni, hasa wanapokutana na hali halisi ya maisha ambayo mara nyingi haitoshelezi matarajio yao. Baada ya miaka ya kujituma masomoni, kukosa ajira au kukabiliana na presha za familia na jamii huwafanya vijana wengi kuhisi mfadhaiko, wasiwasi, na hata msongo wa mawazo. Aidha, ukosefu wa uzoefu wa kukabiliana na changamoto za kifedha, mahusiano, na maisha ya kujitegemea huongeza mzigo wa kihisia. Hali hii inaweza kusababisha matatizo ya afya ya akili kama vile huzuni ya kudumu na kupoteza hamu ya kuendelea na juhudi za kujenga maisha yao. Ili kukabiliana na hali hii, vijana wanapaswa kupata msaada wa kisaikolojia, elimu ya kiakili, na kuungwa mkono na familia pamoja na jamii.
HITIMISHO NA MAPENDEKEZO
Changamoto hizi zinahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa serikali, mashirika binafsi, na jamii kwa ujumla. Serikali inaweza kuweka mikakati ya kukuza ajira, kuboresha mitaala ya elimu ili kuendana na mahitaji ya soko, na kutoa ruzuku kwa wajasiriamali vijana. Vilevile, vijana wanapaswa kuwa wabunifu na kutafuta njia mbadala za kujiajiri na kujifunza ujuzi wa ziada. Kwa kushirikiana, tunaweza kuhakikisha kuwa wahitimu wa vyuo wanapata fursa ya kutumia maarifa yao kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na jamii kwa ujumla.