ONGEZEKO LA WATOTO WA MITAANI  

By Jamal H. Maherea

Nanukuhu kutoka tovuti ya Jamii Forum 2022, “Watoto wa mitaani, ni watoto ambao wanaishi mitaani, nje ya makazi ya kawaida. Kempe Ronald Hope, (2005) anatoa maana ya Mtoto wa Mitaani kama ifuatavyo: “Mtoto wa Mtaani, ni msichana au mvulana ambaye hajafikia umri wa utu uzima, ambapo mtaa (ikijumuisha makazi yasiyokaliwa, maeneo yenye mazingira magumu, na kadhalika) umekuwa makazi, na mahali pa kujikimu kimaisha, ambaye hana ulinzi wa kutosha na ambaye haongozwi na watu wazima wenye kuwajibika”.

Ongezeko la watoto wa mitaani ni changamoto kubwa inayowakumba watoto wengi ulimwenguni ikiwemo Tanzania. watoto hawa, ambao wanakosa makazi salama na malezi ya wazazi au walezi, hukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoathiri maisha yao ya kila siku. Watoto wa mitaani ni wale wanaoishi na kufanya kazi katika mazingira hatarishi ya mtaani, hali inayowafanya kuwa katika hatari ya kukosa elimu, afya bora, na fursa ya kujitengenezea maisha yenye mafanikio. Makala hii itachambua sababu zinazochangia ongezeko la watoto wa mitaani nchini Tanzania, athari wanazokabiliana nazo, na kutoa mapendekezo ya namna ya kuwasaidia watoto hawa.

SABABU ZA ONGEZEKO LA WATOTO WA MITAANI

UMASKINI

Umaskini ndio chanzo kikuu cha watoto wengi kujikuta mitaani. Familia maskini hushindwa kumudu mahitaji ya msingi ya watoto kama chakula, mavazi, na elimu. Hali hii huwalazimisha watoto kutafuta njia za kujikimu mitaani. Watoto kutoka familia maskini katika mikoa mbalimbali ikiwemo Singida hukimbilia kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam na Mwanza kwa matumaini ya kupata kipato. Kwa mujibu wa Mama Lily ambaye ni mama mlezi wa kituo cha KINDAI SAFINA Singida, anaeleza baadhi ya watoto waliopo katika kituo hicho cha malezi ni kutokana na changamoto ya umaskini uliopo katika familia zao. Umaskini huo, huwapelekea watoto kutoka katika familia hizo kuanza kuzurura mitaani na wengine kujiingiza katika tabia zisizofaa.

MIGOGORO YA KIFAMILIA VIFO VYA WAZAZI   

Migogoro ya kifamilia, kama vile talaka na ugomvi wa wazazi, huathiri watoto kisaikolojia na mara nyingine kuwaacha bila malezi. Watoto wanaopitia changamoto hizi hukimbilia mitaani kutafuta uhuru au kujitafutia riziki. Kwa mfano, baadhi ya watoto wanaoishi mitaani katika miji ya Dodoma na Singida wamekimbia migogoro ndani ya familia zao. Vifo vya wazazi kutokana na magonjwa kama ukimwi au ajali vimeacha watoto wengi kama yatima, ambao hawana uangalizi wa kifamilia. Watoto hawa, hasa katika mikoa kama Dodoma na Singida, hukosa msaada wa kifedha na kimaadili, na hivyo kulazimika kujikimu mitaani.  Kupitia kituo cha KINDAI SAFINA Singida pamoja na SAVE THE CHILD kilichopo Dodoma wanaeleza kuwa baadhi ya Watoto hukimbia nyumba kutokana na migogoro ya familia inayowajengea uwonga na kuwapelekea kujiingiza katika kundi la Watoto wa mitaani.

ATHARI ZA KUISHI MITAANI KWA WATOTO

KUKOSA ELIMU NA AFYA BORA

Watoto wa mitaani mara nyingi hukosa fursa ya kupata elimu ya msingi na sekondari kutokana na kutokuwa na msaada wa kifedha au wa kifamilia. Hali hii huzuia maendeleo yao ya kitaaluma na kuwapunguzia nafasi za kujiendeleza kiuchumi hapo baadaye. Watoto wa mitaani hukosa lishe bora, malazi salama, na huduma za afya za msingi. Hii inawaweka katika hatari ya kupata magonjwa kama vile utapiamlo, malaria, na maambukizi ya njia ya hewa. Pia, wengi wao hujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na pombe kwa sababu ya mazingira wanayoishi, hali inayozidi kuathiri afya zao. Kupitia kituo cha KINDAI SAFINA Singida Mama Lily amelithibitisha hili kwa kuwa na baadhi ya watoto ambao walikuwa hawafahamu kusoma na kuandika.

KUHARIBIKA KISAIKOLOJIA KUINGIA KWENYE MAKUNDI HATARI

Maisha ya mitaani huathiri afya ya akili ya watoto, na wengi wao hukumbana na msongo wa mawazo na kiwewe kutokana na changamoto wanazopitia kama unyanyasaji, upweke, na kukataliwa na jamii. Watoto wa mitaani wanapokuwa bila mwongozo wa kifamilia wanaweza kujiunga na makundi ya kihalifu, na kujiingiza kwenye uhalifu mdogo au kuathiriwa na magenge yanayohusishwa na vitendo vya uhalifu. Mfano halisi, mkoa wa Singida unakumbwa na tatizo hili la ongezeko la watoto wa mitaa ambao wengi huuishia kuvuta gundi, bangi na uwizi. Baadhi ya wafanyabiashara katika soko kuu la Singida, wanalalamikia sana watu wanaofanya biashara ya kuwauzia gundi baadhi ya watoto wa mitaani. Hali hii inawaweka katika hatari ya kukamatwa na polisi au kujiingiza kwenye mizozo hatarishi.

NAMNA YA KUWASAIDIA WATOTO WA MITAANI

KUWEZESHA FAMILIA MASKINI KUPITIA MISAADA YA KIFEDHA

Misaada ya kifedha kwa familia maskini inaweza kusaidia kupunguza tatizo la watoto wa mitaani. Programu kama TASAF (Tanzania Social Action Fund) zinatoa misaada kwa familia maskini ili kuimarisha hali zao za maisha na kupunguza watoto kutoroka nyumbani. Kupitia misaada ya kifedha, familia zenye hali duni zitaweza kujikwamua katika hali duni ya kimaisha na kuwekeza nguvu pia katika uangalizi wa watoto wao. Hii itachangia zaidi katika kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani kwa kiasi kikubwa.

KUTOA ELIMU NA MAFUNZO YA KUJITEGEMEA

Elimu ni nyenzo muhimu ya kumsaidia mtoto kuondokana na umasikini. Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanaweza kuanzisha programu za mafunzo ya ufundi stadi kwa watoto wa mitaani, kama vile ushonaji, useremala, na uashi. Hii itawasaidia kupata ujuzi wa kujiajiri na kujitegemea.

KAMPENI ZA KUELIMISHA JAMII KUHUSU HAKI ZA WATOTO

Kampeni za kuelimisha jamii kuhusu haki za watoto ni muhimu sana katika kuimarisha ustawi wa watoto na kujenga jamii yenye ufahamu wa majukumu yao katika malezi bora. Kampeni hizi zinalenga kutoa elimu juu ya haki za watoto, kuwahamasisha wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kutimiza wajibu wao katika kuwalinda na kuwaendeleza watoto. Jamii inaweza kushiriki katika kampeni za kuelimisha kuhusu haki za watoto, umuhimu wa kuwalea watoto katika mazingira bora, na kusaidia kupunguza unyanyasaji na unyanyapaa dhidi ya watoto wa mitaani.

Hivyo, ongezeko la watoto wa mitaani nchini Tanzania ni changamoto inayohitaji jitihada za pamoja kutoka kwa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na jamii kwa ujumla. Watoto hawa wanahitaji msaada wa haraka ili kuwapa nafasi ya kuishi maisha yenye matumaini na mustakabali mzuri. Kwa kuweka mipango thabiti na programu za kuwasaidia watoto wa mitaani, Tanzania inaweza kupunguza ongezeko hili na kuwasaidia watoto hawa kutimiza ndoto zao na kuchangia katika maendeleo ya taifa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top